Karibu katika blog yetu tanze safari ya kufanikiwa na kuwa na uhuru wa kifedha

Alhamisi, 10 Novemba 2016

Mambo (4) Ya Kuzingatia ili Ng'ombe Atoe Maziwa Mengi.,,

 
Ng'ombe Mwenye Afya Bora.
      Karibuni tena wapenzi wa ufugaji katika mtandao pendwa,  katika mtiririko wetu wa safari kuelekea katika ufugaji utakaofungua mlango wa uhuru wa kifedha,  ili tuje kufurahia matunda ya ufugaji wetu. Makala haya yatakuwa marefu na nitachambua kwa kina mambo mbalimbali muhimu, kwa sababu madhumuni makubwa katika kufuga ng'ombe wa maziwa ni kupata maziwa mengi na bora.  Ni muda mzuri sasa tupambane ili kuachana na ufugaji wa mazoe tufuge kwa tija,  leo tuangazie mambo manne ambayo kama tukiyazingatia vizuri ni lazima tutafanikiwa na kufikia malengo yetu tuliyojiwekea.
 Wafugaji wapendwa, katika makala zilizopita
nimezunguzia sana jinsi ya kuepukana na ufugaji wa mazoea ambao unatutesa na kutuburuza kuelekea katika umaskini kila inapoitwa leo.  katika makala zilizopita nilishauri baadhi ya mambo ambayo tukiyatimiza ni lazima tutafanikiwa,  jaribu kupitia makala hizo kwa utulivu halafu uyafanyie kazi mambo yote yaliyomo,  nina amini utaanza kuona mwanga mbele yako.  Basi leo tuangazie haya mambo manne ambayo kama tutayazingatia ni lazima tupate maziwa mengi na bora kutoka kwa ng'ombe wale wale uliozoea kuwafuga kwa kutofuata kanuni bora za ufugaji.
Ng'ombe Wenye Afya Bora.
  
Ng'ombe Wenye Afya Bora.
     Jambo la kwanza kabisa kuzingatia ni Afya ya ng'ombe mwenyewe,  tunapozungumzia habari ya Afya ya ng'ombe tunalenga katika mabo mengi,  ng'ombe anae andamwa na magojwa mara kwa mara tunasema ng'ombe huyu hana afya nzuri,  kwa hiyo mfugaji anatakiwa ahakikishe kuwa ng'ombe wake anakuwa na afya njema wakati wote,  ninashauri kuwa ili uweze kuhakikisha kuwa ng'ombe wako anakuwa na afya njema wakati wote ni lazima uwe na daktari wa mifugo atakaye kuwa anapatikana kuhudumia mifugo yako wakati wote,  daktari huyu unatakiwa kujenga nae urafiki wa kudumu,  ikiwezekana mnakuwa kama ndugu kabisa,  hii maana yake ni kwamaba,  mkishakuwa marafiki mnakuwa na tabia ya kutembeleana,  na akikutembelea hata kama hakuna tatizo katika mifugo yako ni lazima ataikagua na kudodosa kama kuna tatizo ili aweze kulitatua au kukupa maelekezo ya msingi kwa mambo yale yatakayo kuwa hayajakaa vizuri,  au atakupa moyo kwa mambo yale atakayoona kuwa unafanya vizuri,  ukitiwa moyo unapata faraja na ni lazima utaongeza bidii katika kufanya vizuri zaidi.
Daktari Wa Mifugo.
               Ukijenga urafiki mzuri na daktari utapata faida nyingi sana,  kuna baadhi ya matibabu madogo madogo ambayo mkulima anaweza kuyafanya vizuri bila kuhitaji msaada wa daktari,  kwa mfano daktari akishakufundisha vipimo na jinsi ya kuwapa mifugo yako chanjo mbalimbali na daktari akajiridhisha kuwa umeshaelewa vizuri,  basi atakuruhusu uendelee kutoa chanjo hizo kipindi ambacho atakuwa mbali na mradi wako,  maana kuna dawa za chanjo ambazo hutolewa kwa wanyama kila baada ya muda fulani,  dawa hizi nazo unaweza kuwa unatoa chanjo kila muda wake ukifika(hii ni baada ya rafiki yako daktari kuwa ameshakufundisha na kuridhika kuwa umeshaelewa vya kutosha).
              Baadhi ya dawa zinakuwa na maelekezo ya matumizi yake,  vipimo na kadhalka,  nashauri kuwa ni lazima upate maelezo ya kina juu ya matumizi ya dawa hizo kutoka kwa daktari wako,  kuna baadhi ya vitu vidogo vidogo kama kupaka dawa za kuzuia wadudu ,  kuwaogesha ng'ombe na mambo mengine kama usafi unaweza kuyafanya kwa kupata uzoefu kwa kujifunza taratibu shamabani kwako.
              Nimezungumzia habari ya daktari na juu ya kujenga urafiki na daktari kwa sababu baadhi ya wafugaji wa mazoea wamekuwa na tabia ya kutotilia maanani umuhimu wa daktari,  hili ni jambo hatari sana kwa mfugaji anaetaka kufuga na kufanikiwa katika ufugaji wake,  mfugaji kujifanya unajua kila kitu ni makosa makubwa,  ili kufikia lengo la kupata maziwa mengi na bora,  umuhimu wa daktari katika mradi ni wa lazima.  Ndiyo maana nikashauri njia nzuri ya kufanya ufanikiwe ni kujenga urafiki mzuri na wa kudumu na daktari wa mifugo yako,  sasa hapa mfugaji unakuwa na uhakika wa afya ya mwili wa ng'ombe wako,  kwa maana sasa kwa kushirikiana na mtaalam daktari wa mifugo yako itakuwa salama mbali na magojwa mbalimbali.
               Wanyama wako wakishakuwa na Afya njema,  sasa unakuwa tayari umeshafungua mlango mmoja kati ya milango minne kuelekea katika kupata maziwa mengi na bara.  Jambo la pili ambalo ni muhimu sana ni mazingira atakayoishi ng'ombe mwenyewe,  ili ng'ombe aweze kufikia katika kilele cha utoaji maziwa mengi na bora,  ng'ombe huyu anahitaji mazingira safi,  tulivu na salama . Banda la ng'ombe linatakiwa lijengwe kitaalam ili ngombe aweze kuishi kwa starehe,  kama binadamu unavyohitaji kishi sehemu nzuri na salama,  wanyama pia wanahitaji mazingira kama hayo,  banda la ngombe lijengwe kwa maelekezo maalum toka kwa mtaalam wa ujenzi wa mabanda ya wanyama.
Banda Bora La Ng'ombe.
                  Banda liwe na nafasi  ya kutosha, pia  hewa ya kutosha ipatikane ndani bila shida yoyote,  kusiwe na joto kali bandani,  banda lijengwe katika hali ambayo usafi utaweza kufanyika kwa urahisi,  mkojo uweze kutiririka wenyewe hadi nje bila kuhitaji kusukumwa,  hapa mwinuko kiasi fulani unahitajika kama atakavyoelekeza mtaalam wa ujenzi,   banda linatakiwa lijengwe sehemu tulivu pasipoweza kufikiwa na makelele mengi,  mbali na vuruguvurugu,  ndani ya banda mahali pa kulala pawe pazuri,  sakafu laini,  patandazwe majani makavu na laini.
               Usafi wa mara kwa mara bandani ni muhimu sana,    ili ng'ombe akae mahali pasafi pakavu pasipokuwa na harufu mbaya itakayo mkera ngombe wakati wote.  kama kutakuwa na eneo la kumfungulia ngombe wakati wa mchana,  basi eneo hilo nalo liwe salama,  ni lazima ujenge uzio utakao mkinga ngombe asitoroke au kufikiwa kwa urahisi na watu wabaya.  Ni lazima mfugaji ujiridhishe na usalama wa ngombe wako muda wote atakaokuwa nje ya banda lake.  Ulinzi kwa maana ya kuwepo mtu wa kumchunga muda wote ni lazima,  siku hizi kumekuwepo na taarifa nyingi za ngombe kuibiwa, kuna wezi stadi siku hizi,  ngombe wako akipotea muda wa nusu saa ni mwingi,  utakachoambulia kama hajaondoka mzima mzima ni ngozi, kichwa, makanyagio na utumbo.
                 Hivi ninavyoandika hapa huenda kuna mtu yamlifika siku sii nyingi,  balaa hili limeshawakumba watu wengi hapa mjini na kwingineko.  Mbali na hilo kuna tabia ya watu kuwapiga ngombe kwa mawe hata wakati mwingine kuwadhuru kwa vitu vyenye ncha kali kwa makusudi tu ili kufurahia ngombe atakavyo umia au penginepo kukutia wewe mfugaji hasara makusudi.  Ngombe ni kiwanda chako cha kukuzalishia pesa,  kiwanda chochote lazima kiwe na ulinzi muda wote.
         
Majani Ya Ng'ombe(Umburi Fodders).
      Jambo la tatu baada ya kujiridhisha na afya na mazingira bora ya ngombe kuishi ni LISHE,  jambo hili ndiyo Dira itakayo kuonyesha njia kamili ya kufikia mafanikio na matarajio yako yote ya ufugaji,  hapa ndipo penye njia panda kwa mfugaji,  katika safari yoyote ni lazima utafika njia panda,  ili uweze kufika salama na haraka uendako ni lazima ujue ukifika njia panda uwe na uhakika na uelekeo sahihi,  basi safari yako inakuwa nyepesi sana.  Hapa nina maanisha kuwa ni lazima ng'ombe wako apate mlo kamili,  katika makala iliyopita niliangazia kwa ufupi kipengele hiki,   hivyo unaweza kupitia kwa wakati wako makala hiyo mwenyewe.  Ng'ombe anatakiwa kupatiwa chakula bora na cha kutosha,   kwa wale wanaofuga kwa mazoea wamekuwa na desturi ya kuwalisha ng'ombe chakula kile kinachopatikana kwa siku hiyo,  yakipatikana majani kidogo sawa, yakipatikana mengi sawa,  ilimradi kumetupiwa chakula horini mwa ng'ombe,  kwa mtindo huu ni hakika kuwa hatutafika popote.
   
Fodder Ya Mahindi(Umburi Fodders).
       Ng'ombe anatakiwa kupatiwa majani ya kutosha,  chakula kikuu cha ngombe ni majani machanga mabichi, yawe ya  kijani kibichi kabisa,   viini lishe muhimu sana kwa ng'ombe vinapatikana katika kijani kibichi na kichanga, ng'ombe apatiwe majani yenye uzito sawa na sehemu ya kumi ya uzito wake,  kwa mfano kama ng'ombe ana uzito wa kilo 450,  basi ni lazima alishwe kilo 45 za majani au zaidi kwa kadri atakavyoweza kula kila siku, ila isiwe pungufu ya uzito huo.  Majani yako ya aina nyigi kutegemea na eneo,  kwa mfano kuna sehemu zinazopata mvua za kutosha kwa kipindi kerefu cha mwaka,  majani yanakuwa mengi na ya kutosha,  kuna majani kama Steria,  elephant grass,   matete, majani ya migomba pamoja na mashina yake,  ukoka na kadhalka,  inashauriwa kuwapatia ngombe majani yenye virutubisho vingi kama Lucina na majani ya Mlonge,  yapo ya kuotesha kama Steria , Elephant grass, Matete,  na Hydroponic fodders tokana na nafaka mbalimbali,  yapo yanayomea maporini na kadhalka, vyovyote vile utakavyoweza kuyapata, ila yawe masafi na salama.
         
Majani Bora Ya Mifugo.
  Ngombe anatakiwa alishwe kwa kipimo maalum, chakula apewe kulingana na uzito wake,  na hii ni KANUNI au tumezoea kusema  ni SHERIA ambayo ni ya msingi na haitakiwi kukiukwa,  ukiikiuka kanuni hii na kufuata nyingine zote kwa ukamilifu,  bado hutapata matokeo yoyote ya maanana,  na hili linatakiwa litimizwe siku zote,  ndio maana katika makala zilizotangulia nilisisitiza juu ya kuwepo bajeti inayojitosheleza kulingana na ukubwa wa mradi tuliopanga kuwa nao,  ni bora ukaahirisha kuanza mradi kuliko kukimbilia kuanzisha mradi usiokuwa na uhakika wa bajeti ya KUDUMU ya kuendesha mradi wenyewe.
              UBAHILI ni janga jingine linalofanya tushindwe kufanikiwa katika mambo mengi tunayopanga kuyafanya.  Maana utakuta bajeti ya kuendesha mradi iko vizuri sana,  lakini utakuta badala ya mfugaji kununua vitu vilivyo katika viwango, utakuta anafanya vitu duni kuanzia kununua ngombe mwenyewe,  kumjengea banda lisilokidhi viwango,  kuto kumpatiang'ombe  huduma bora,  kuwalisha vyakula vya hovyohovyo!
             
Majani Makavu Kiasi Ni Lazima Kwa Afya ya ng'ombe.
   Jambo lililo ufunguo wa kufungua mlango wa nne ili kuelekea katika kupata maziwa mengi na bara ni kuwa na RATIBA ya kumhudumia ng'ombe na ratiba ifuatwe kikamilifu,  kufuata ratiba kutamfanya ng'ombe aitambue ratiba yake,  hii kitaalam ni muhimu kwa sababu kwa ng'ombe akishaijua ratiba yake atakuwa anafanya maandalizi kujiandaa kwa kila jambo litakalokuwa linafuatia.  Kwa mfano ratiba inaanza asubuhi saa kumi na mbili kamili,  ratiba ianze kwa kukamua maziwa,  wakati wa kukamua maziwa unashauriwa kumpatia ng'ombe chakuala anachokipenda kuliko vingine, awe anakula wakati zoezi la kukamua maziwa likiendelea,  na mara nyingi inakuwa ni kile chakula chenye mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali,  mparazo wa mahindi,  ngano au shayiri,  mashudu ya pamba,  mashudu ya alizeti,  soya,   chumvi,  pamoja na mchanganyiko wa madini mbalimbali ambayo ni pamoja na Probiotic powder ambayo ni muhimu sana kwa kusaidia mfumo wa chakula kumeng'enywa vizuri tumboni mwa ng'ombe.
               Nimekuwa nikiandika mchanganyiko wa madini bila kufafanua kwa undani, kuna makala itafuata kuzungumzia kwa undani mchanganyiko huu na umuhimu wake kwa mifugo,  mchanganyiko wa madini katika viwango sahihi ni muhimu sana sana katika upatikanaji wa maziwa mengi na bora, wakati ng'ombe akifurahia ulaji wa chakula hiki kitamu anachokipenda,  ndipo sasa atakapo jisikia raha,  na kukupatia wewe maziwa mengi ya kutosha,  kama utaweza kumpigia na mziki laini kwa mluzi wa kifugaji itakuwa bora zaidi,  zoezi la kukamua lifanyike kwa utulivu,  simamisha pilikapilika nyingine zote katika banda,  pilikapilika nyingi zitamwondoa ng'ombe katika mtiririko wa kuandaa na kuachia maziwa.
         
Mashine Ya Kukamulia Maziwa Ya Ng'ombe.
    Kuna jambo moja mhimu unalotakiwa kujua katika kipengele hiki cha ukamuaji wa maziwa, kwamba  ng'ombe huwa anatengeneza maziwa wakati ule ule anapokamuliwa,  hakuna mahali maziwa yanapojikusanya ndio yatokee hapo wakati wa kukamualiwa,  hata ukimchinja ngombe aliyetakiwa kukamuliwa lita ishirini za maziwa muda mfupi kabla ya kukamuliwa,  hutakuta maziwa yoyote ndani ya mwali wa ng'ombe.
                 Mpaka hapa utakuwa umejifunza kitu fulani muhimu,  baada ya kukamua,  ratiba iendelee labda kwa kumpa ng'ombe maji ya kutosha ili kufidia kiasi cha maji yaliyopotea mwilini mwake wakati wa kukamua maziwa,  baada ya hapo unaweza kufanya usafi wa jumla bandani maana utakuwa ulifanya usafi kidogo kuandaa sehemu ya kukamulia maziwa.  Ratiba iendelee kwa mpangilio maalum hadi ng'ombe atakapolala usiku.  kwamba,  kama ng'ombe anakamuliwa saa kumi na mbili kamili asubuhi,  basi zoezi hilo lifanyike muda huo huo siku zote bila kukosea,  usijiulize maswali mengi,  kwamba ng'ombe na kusoma saa wapi na wapi,  hapo utakuwa unakosea, hapa falsafa ya HISIA inafanya kazi.
Kukamua Maziwa Kwa mikono.
                Zingatia usafi wakati wa kukamua maziwa,  kiwele cha ng'ombe kisafishwe kwa maji ya uvuguvugu, yasiwe ya moto sana au ya baridi sana, maji ya vuguvugu yanamsisimua ng'ombe, hivyo kumfanya aachie maziwa yatoke kwa wingi na urahisi,  tumia sabuni maalumu kusafishia kiwele cha ng'ombe hadi uchafu wote utoke,  suuza vizuri kuhakikisha harufu na mabaki ya sabuni yametoweka,  kausha kiwele kwa kutumia taulo maalum,  kama unakamua kwa kutumia mikono unashauriwa kutumia mafuta maalum ya kulainisha chuchu za ng'ombe ili ng'ombe asipate maumivu au kuchubuka wakati wa kukamua, hakikisha ng'ombe hapati misukosuko yoyote wakati huu ili asikie raha aachie maziwa ya kutosha.Usafi wakati wa kukamua ni muhimu ili maziwa yawe ya kiwango kinachotakiwa kama tulivyoangazia katika makala zilizopiata.
 
Kukamua Maziwa Kwa Kutumia Mashine.
         Vyombo vya kukamulia na kuhifadhia maziwa viwe safi na maalum kwa ajili ya maziwa, utavipata katika maduka ya kuuzia madawa ya kilimo na mifugo, kampuni yetu itakuwa inajishughulisha na uuzaji wa vifaa vyote muhimu katika tasnia hii, mashine za kukamulia maziwa za ukubwa mbalimbali, kila mfugaji aweze kujipatia vifaa kulingana na ukubwa wa mradi wake.
              Kufika hapa tunafikia tamati ya makala yetu ya leo, nikushukuru sana kwa uvumilivu wako wa kupitia makala haya kipengele baada ya kipengele,  niimani yangu kuwa umepata kitu cha kukufanya ubadili au uboreshe zaidi mradi wako,  nakukaribisha katika makala nzuri zinazofuata muda sii mrefu,  nakuomba sana usiache kuandika maoni yako ambayo ninaamini yatasaidia na knitia moyo katika safari yetu ya matumaini.
                NAKUTAKIA BARAKA ZA MUNGU NA ULINZI WAKE POPOTE ULIPO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni