|
Ng'ombe Mwenye Afya Bora. |
Karibuni tena wapenzi wa ufugaji katika mtandao pendwa, katika mtiririko
wetu wa safari kuelekea katika ufugaji utakaofungua mlango wa uhuru wa
kifedha, ili tuje kufurahia matunda ya ufugaji wetu. Makala haya
yatakuwa marefu na nitachambua kwa kina mambo mbalimbali muhimu, kwa
sababu madhumuni makubwa katika kufuga ng'ombe wa maziwa ni kupata
maziwa mengi na bora. Ni muda mzuri sasa tupambane ili kuachana na
ufugaji wa mazoe tufuge kwa tija, leo tuangazie mambo manne ambayo kama
tukiyazingatia vizuri ni lazima tutafanikiwa na kufikia malengo yetu
tuliyojiwekea.
Wafugaji wapendwa, katika makala zilizopita
nimezunguzia
sana jinsi ya kuepukana na ufugaji wa mazoea ambao unatutesa na
kutuburuza kuelekea katika umaskini kila inapoitwa leo. katika makala
zilizopita nilishauri baadhi ya mambo ambayo tukiyatimiza ni lazima
tutafanikiwa, jaribu kupitia makala hizo kwa utulivu halafu uyafanyie
kazi mambo yote yaliyomo, nina amini utaanza kuona mwanga mbele yako.
Basi leo tuangazie haya mambo manne ambayo kama tutayazingatia ni
lazima tupate maziwa mengi na bora kutoka kwa ng'ombe wale wale uliozoea
kuwafuga kwa kutofuata kanuni bora za ufugaji.
|
Ng'ombe Wenye Afya Bora. |
|
Ng'ombe Wenye Afya Bora. |
Jambo la kwanza kabisa
kuzingatia ni Afya ya ng'ombe mwenyewe, tunapozungumzia habari ya Afya
ya ng'ombe tunalenga katika mabo mengi, ng'ombe anae andamwa na magojwa
mara kwa mara tunasema ng'ombe huyu hana afya nzuri, kwa hiyo mfugaji
anatakiwa ahakikishe kuwa ng'ombe wake anakuwa na afya njema wakati
wote, ninashauri kuwa ili uweze kuhakikisha kuwa ng'ombe wako anakuwa na
afya njema wakati wote ni lazima uwe na daktari wa mifugo atakaye kuwa
anapatikana kuhudumia mifugo yako wakati wote, daktari huyu unatakiwa
kujenga nae urafiki wa kudumu, ikiwezekana mnakuwa kama ndugu kabisa,
hii maana yake ni kwamaba, mkishakuwa marafiki mnakuwa na tabia ya
kutembeleana, na akikutembelea hata kama hakuna tatizo katika mifugo
yako ni lazima ataikagua na kudodosa kama kuna tatizo ili aweze
kulitatua au kukupa maelekezo ya msingi kwa mambo yale yatakayo kuwa
hayajakaa vizuri, au atakupa moyo kwa mambo yale atakayoona kuwa
unafanya vizuri, ukitiwa moyo unapata faraja na ni lazima utaongeza
bidii katika kufanya vizuri zaidi.
|
Daktari Wa Mifugo. |
Ukijenga urafiki mzuri na daktari utapata faida nyingi sana, kuna
baadhi ya matibabu madogo madogo ambayo mkulima anaweza kuyafanya
vizuri bila kuhitaji msaada wa daktari, kwa mfano daktari
akishakufundisha vipimo na jinsi ya kuwapa mifugo yako chanjo mbalimbali
na daktari akajiridhisha kuwa umeshaelewa vizuri, basi atakuruhusu
uendelee kutoa chanjo hizo kipindi ambacho atakuwa mbali na mradi wako,
maana kuna dawa za chanjo ambazo hutolewa kwa wanyama kila baada ya
muda fulani, dawa hizi nazo unaweza kuwa unatoa chanjo kila muda wake
ukifika(hii ni baada ya rafiki yako daktari kuwa ameshakufundisha na
kuridhika kuwa umeshaelewa vya kutosha).
Baadhi ya dawa zinakuwa na maelekezo ya matumizi yake, vipimo na
kadhalka, nashauri kuwa ni lazima upate maelezo ya kina juu ya matumizi
ya dawa hizo kutoka kwa daktari wako, kuna baadhi ya vitu vidogo vidogo
kama kupaka dawa za kuzuia wadudu , kuwaogesha ng'ombe na mambo mengine
kama usafi unaweza kuyafanya kwa kupata uzoefu kwa kujifunza taratibu
shamabani kwako.
Nimezungumzia habari ya daktari na juu ya kujenga
urafiki na daktari kwa sababu baadhi ya wafugaji wa mazoea wamekuwa na
tabia ya kutotilia maanani umuhimu wa daktari, hili ni jambo hatari sana
kwa mfugaji anaetaka kufuga na kufanikiwa katika ufugaji wake, mfugaji
kujifanya unajua kila kitu ni makosa makubwa, ili kufikia lengo la
kupata maziwa mengi na bora, umuhimu wa daktari katika mradi ni wa
lazima.
Ndiyo maana nikashauri njia nzuri ya kufanya ufanikiwe ni kujenga
urafiki mzuri na wa kudumu na daktari wa mifugo yako, sasa hapa mfugaji
unakuwa na uhakika wa afya ya mwili wa ng'ombe wako, kwa maana sasa kwa
kushirikiana na mtaalam daktari wa mifugo yako itakuwa salama mbali na
magojwa mbalimbali.
Wanyama wako wakishakuwa na Afya njema, sasa unakuwa tayari
umeshafungua mlango mmoja kati ya milango minne kuelekea katika kupata
maziwa mengi na bara.
Jambo la pili ambalo ni muhimu sana ni mazingira atakayoishi
ng'ombe mwenyewe, ili ng'ombe aweze kufikia katika kilele cha utoaji
maziwa mengi na bora, ng'ombe huyu anahitaji mazingira safi, tulivu na
salama . Banda la ng'ombe linatakiwa lijengwe kitaalam ili ngombe aweze
kuishi kwa starehe, kama binadamu unavyohitaji kishi sehemu nzuri na
salama, wanyama pia wanahitaji mazingira kama hayo, banda la ngombe
lijengwe kwa maelekezo maalum toka kwa mtaalam wa ujenzi wa mabanda ya
wanyama.
|
Banda Bora La Ng'ombe. |
Banda liwe na nafasi ya kutosha, pia hewa ya kutosha ipatikane ndani bila shida yoyote,
kusiwe na joto kali bandani, banda lijengwe katika hali ambayo usafi
utaweza kufanyika kwa urahisi, mkojo uweze kutiririka wenyewe hadi nje
bila kuhitaji kusukumwa, hapa mwinuko kiasi fulani unahitajika kama
atakavyoelekeza mtaalam wa ujenzi, banda linatakiwa lijengwe sehemu
tulivu pasipoweza kufikiwa na makelele mengi, mbali na vuruguvurugu,
ndani ya banda mahali pa kulala pawe pazuri, sakafu laini, patandazwe
majani makavu na laini.
Usafi wa mara kwa mara bandani ni muhimu sana,
ili ng'ombe akae mahali pasafi pakavu pasipokuwa na harufu mbaya itakayo
mkera ngombe wakati wote.
kama kutakuwa na eneo la kumfungulia ngombe wakati wa mchana,
basi eneo hilo nalo liwe salama, ni lazima ujenge uzio utakao mkinga
ngombe asitoroke au kufikiwa kwa urahisi na watu wabaya. Ni lazima
mfugaji ujiridhishe na usalama wa ngombe wako muda wote atakaokuwa nje
ya banda lake. Ulinzi kwa maana ya kuwepo mtu wa kumchunga muda wote ni
lazima, siku hizi kumekuwepo na taarifa nyingi za ngombe kuibiwa, kuna
wezi stadi siku hizi, ngombe wako akipotea muda wa nusu saa ni mwingi,
utakachoambulia kama hajaondoka mzima mzima ni ngozi, kichwa, makanyagio
na utumbo.
Hivi ninavyoandika hapa huenda kuna mtu yamlifika siku sii nyingi,
balaa hili limeshawakumba watu wengi hapa mjini na kwingineko. Mbali na
hilo kuna tabia ya watu kuwapiga ngombe kwa mawe hata wakati mwingine
kuwadhuru kwa vitu vyenye ncha kali kwa makusudi tu ili kufurahia ngombe
atakavyo umia au penginepo kukutia wewe mfugaji hasara makusudi. Ngombe
ni kiwanda chako cha kukuzalishia pesa, kiwanda chochote lazima kiwe na
ulinzi muda wote.
|
Majani Ya Ng'ombe(Umburi Fodders). |
Jambo la tatu baada ya kujiridhisha na afya na mazingira bora ya
ngombe kuishi ni LISHE, jambo hili ndiyo Dira itakayo kuonyesha njia
kamili ya kufikia mafanikio na matarajio yako yote ya ufugaji, hapa
ndipo penye njia panda kwa mfugaji, katika safari yoyote ni lazima
utafika njia panda, ili uweze kufika salama na haraka uendako ni lazima
ujue ukifika njia panda uwe na uhakika na uelekeo sahihi, basi safari
yako inakuwa nyepesi sana. Hapa nina maanisha kuwa ni lazima ng'ombe wako
apate mlo kamili, katika makala iliyopita niliangazia kwa ufupi
kipengele hiki, hivyo unaweza kupitia kwa wakati wako makala hiyo
mwenyewe.
Ng'ombe anatakiwa kupatiwa chakula bora na cha kutosha, kwa wale
wanaofuga kwa mazoea wamekuwa na desturi ya kuwalisha ng'ombe chakula
kile kinachopatikana kwa siku hiyo, yakipatikana majani kidogo sawa,
yakipatikana mengi sawa, ilimradi kumetupiwa chakula horini mwa ng'ombe,
kwa mtindo huu ni hakika kuwa hatutafika popote.
|
Fodder Ya Mahindi(Umburi Fodders). |
Ng'ombe anatakiwa kupatiwa majani ya kutosha, chakula kikuu cha ngombe
ni majani machanga mabichi, yawe ya kijani kibichi kabisa, viini lishe
muhimu sana kwa ng'ombe vinapatikana katika kijani kibichi na kichanga, ng'ombe
apatiwe majani yenye uzito sawa na sehemu ya kumi ya uzito wake, kwa
mfano kama ng'ombe ana uzito wa kilo 450, basi ni lazima alishwe kilo 45
za majani au zaidi kwa kadri atakavyoweza kula kila siku, ila isiwe pungufu ya
uzito huo.
Majani yako ya aina nyigi kutegemea na eneo, kwa mfano kuna sehemu
zinazopata mvua za kutosha kwa kipindi kerefu cha mwaka, majani
yanakuwa mengi na ya kutosha, kuna majani kama Steria, elephant grass,
matete, majani ya migomba pamoja na mashina yake, ukoka na kadhalka, inashauriwa kuwapatia ngombe majani yenye
virutubisho vingi kama Lucina na majani ya Mlonge, yapo ya kuotesha kama Steria , Elephant grass, Matete, na Hydroponic fodders tokana na nafaka mbalimbali,
yapo yanayomea maporini na kadhalka, vyovyote vile utakavyoweza
kuyapata, ila yawe masafi na salama.
|
Majani Bora Ya Mifugo. |
Ngombe anatakiwa alishwe kwa kipimo
maalum, chakula apewe kulingana na uzito wake, na hii ni KANUNI au
tumezoea kusema ni SHERIA ambayo ni ya msingi na haitakiwi kukiukwa,
ukiikiuka kanuni hii na kufuata nyingine zote kwa ukamilifu, bado
hutapata matokeo yoyote ya maanana, na hili linatakiwa litimizwe siku
zote, ndio maana katika makala zilizotangulia nilisisitiza juu ya kuwepo
bajeti inayojitosheleza kulingana na ukubwa wa mradi tuliopanga kuwa
nao, ni bora ukaahirisha kuanza mradi kuliko kukimbilia kuanzisha mradi
usiokuwa na uhakika wa bajeti ya KUDUMU ya kuendesha mradi wenyewe.
UBAHILI ni janga jingine linalofanya tushindwe kufanikiwa katika
mambo mengi tunayopanga kuyafanya. Maana utakuta bajeti ya kuendesha
mradi iko vizuri sana, lakini utakuta badala ya mfugaji kununua vitu
vilivyo katika viwango, utakuta anafanya vitu duni kuanzia kununua ngombe
mwenyewe, kumjengea banda lisilokidhi viwango, kuto kumpatiang'ombe huduma
bora, kuwalisha vyakula vya hovyohovyo!
|
Majani Makavu Kiasi Ni Lazima Kwa Afya ya ng'ombe. |
Jambo lililo ufunguo wa kufungua mlango wa nne ili kuelekea
katika kupata maziwa mengi na bara ni kuwa na RATIBA ya kumhudumia
ng'ombe na ratiba ifuatwe kikamilifu, kufuata ratiba kutamfanya ng'ombe
aitambue ratiba yake, hii kitaalam ni muhimu kwa sababu kwa ng'ombe
akishaijua ratiba yake atakuwa anafanya maandalizi kujiandaa kwa kila
jambo litakalokuwa linafuatia. Kwa mfano ratiba inaanza asubuhi saa kumi
na mbili kamili, ratiba ianze kwa kukamua maziwa, wakati wa kukamua
maziwa unashauriwa kumpatia ng'ombe chakuala anachokipenda kuliko
vingine, awe anakula wakati zoezi la kukamua maziwa likiendelea, na mara nyingi inakuwa ni kile chakula chenye mchanganyiko wa
virutubisho mbalimbali, mparazo wa mahindi, ngano au shayiri, mashudu ya
pamba, mashudu ya alizeti, soya, chumvi, pamoja na mchanganyiko wa
madini mbalimbali ambayo ni pamoja na Probiotic powder ambayo ni muhimu
sana kwa kusaidia mfumo wa chakula kumeng'enywa vizuri tumboni mwa
ng'ombe.
Nimekuwa nikiandika mchanganyiko wa madini bila kufafanua kwa undani, kuna makala itafuata
kuzungumzia kwa undani mchanganyiko huu na umuhimu wake kwa mifugo,
mchanganyiko wa madini katika viwango sahihi ni muhimu sana sana katika
upatikanaji wa maziwa mengi na bora, wakati ng'ombe akifurahia ulaji wa
chakula hiki kitamu anachokipenda, ndipo sasa atakapo jisikia raha, na
kukupatia wewe maziwa mengi ya kutosha, kama utaweza kumpigia na mziki
laini kwa mluzi wa kifugaji itakuwa bora zaidi, zoezi la kukamua
lifanyike kwa utulivu, simamisha pilikapilika nyingine zote katika
banda, pilikapilika nyingi zitamwondoa ng'ombe katika mtiririko wa
kuandaa na kuachia maziwa.
|
Mashine Ya Kukamulia Maziwa Ya Ng'ombe. |
Kuna jambo moja mhimu unalotakiwa kujua katika kipengele hiki cha
ukamuaji wa maziwa, kwamba ng'ombe huwa anatengeneza maziwa wakati ule ule
anapokamuliwa, hakuna mahali maziwa yanapojikusanya ndio yatokee hapo
wakati wa kukamualiwa, hata ukimchinja ngombe aliyetakiwa kukamuliwa
lita ishirini za maziwa muda mfupi kabla ya kukamuliwa, hutakuta maziwa
yoyote ndani ya mwali wa ng'ombe.
Mpaka hapa utakuwa umejifunza kitu fulani muhimu, baada ya kukamua,
ratiba iendelee labda kwa kumpa ng'ombe maji ya kutosha ili kufidia
kiasi cha maji yaliyopotea mwilini mwake wakati wa kukamua maziwa, baada
ya hapo unaweza kufanya usafi wa jumla bandani maana utakuwa ulifanya
usafi kidogo kuandaa sehemu ya kukamulia maziwa. Ratiba iendelee kwa
mpangilio maalum hadi ng'ombe atakapolala usiku. kwamba, kama ng'ombe
anakamuliwa saa kumi na mbili kamili asubuhi, basi zoezi hilo lifanyike
muda huo huo siku zote bila kukosea, usijiulize maswali mengi, kwamba
ng'ombe na kusoma saa wapi na wapi, hapo utakuwa unakosea, hapa falsafa
ya HISIA inafanya kazi.
|
Kukamua Maziwa Kwa mikono. |
Zingatia usafi wakati wa kukamua maziwa, kiwele cha ng'ombe
kisafishwe kwa maji ya uvuguvugu, yasiwe ya moto sana au ya baridi sana, maji ya vuguvugu yanamsisimua ng'ombe, hivyo kumfanya aachie maziwa yatoke kwa wingi na urahisi,
tumia sabuni maalumu kusafishia kiwele cha ng'ombe hadi uchafu wote
utoke, suuza vizuri kuhakikisha harufu na mabaki ya sabuni yametoweka,
kausha kiwele kwa kutumia taulo maalum, kama unakamua kwa kutumia mikono
unashauriwa kutumia mafuta maalum ya kulainisha chuchu za ng'ombe ili
ng'ombe asipate maumivu au kuchubuka wakati wa kukamua, hakikisha ng'ombe
hapati misukosuko yoyote wakati huu ili asikie raha aachie maziwa ya
kutosha.Usafi wakati wa kukamua ni muhimu ili maziwa yawe ya kiwango
kinachotakiwa kama tulivyoangazia katika makala zilizopiata.
|
Kukamua Maziwa Kwa Kutumia Mashine. |
Vyombo vya kukamulia na kuhifadhia maziwa viwe safi na maalum kwa ajili ya maziwa, utavipata katika maduka ya kuuzia madawa ya kilimo na mifugo, kampuni yetu itakuwa inajishughulisha na uuzaji wa vifaa vyote muhimu katika tasnia hii, mashine za kukamulia maziwa za ukubwa mbalimbali, kila mfugaji aweze kujipatia vifaa kulingana na ukubwa wa mradi wake.
Kufika hapa tunafikia tamati ya makala yetu ya leo, nikushukuru sana kwa uvumilivu wako wa kupitia makala haya kipengele baada ya kipengele, niimani yangu kuwa umepata kitu cha kukufanya ubadili au uboreshe zaidi mradi wako, nakukaribisha katika makala nzuri zinazofuata muda sii mrefu, nakuomba sana usiache kuandika maoni yako ambayo ninaamini yatasaidia na knitia moyo katika safari yetu ya matumaini.
NAKUTAKIA BARAKA ZA MUNGU NA ULINZI WAKE POPOTE ULIPO.