Karibu katika blog yetu tanze safari ya kufanikiwa na kuwa na uhuru wa kifedha

Jumatatu, 31 Oktoba 2016

Chakula Bora Kwa Ng'ombe wa Maziwa.

NG'OMBE BORA WA MAZIWA.
          Karibu ndugu msomaji wa Blog pendwa na wafugaji na wasio wafugaji, leo tutaangazia juu ya umuhimu wa kuwapa ng'ombe wetu chakula bora na chenye virutubisho vyote ili tuweze kupata maziwa mengi na bora kabisa. Maziwa bora ni yale  yaliyotimia katika uhalisia wa maziwa, ukianzia na ladha, rangi na virutubisho kamili vinavyotakiwa kuwepo katika maziwa, pia maziwa yanatakiwa yawe na harufu nzuri.  Kuyapata haya yote unatakiwa kukidhi vigezo vingi, ikiwa ni pamoja jamii ya ng'ombe utakayokuwa umemchagua, katika makala zitakazofuata tutaangazia aina za jamii za ng'ombe wanaoweza kufugwa katika kanda mbalimbali, ubora wa faida na hasara na mambo mengine yatakayotusaidia kuchagua jamii  inayofaa katika ukanda tuliopo. Ubora wa maziwa unatakiwa uzingatiwe muda wote wa ufugaji, kwa maana kwamba isiwe juma hili maziwa yanakuwa bora na juma linalofuatia maziwa kutoka katika shamba lako yanakuwa vinginevyo.
NG'OMBE BORA WA MAZIWA.
           Jambo hili linatakiwa kuepukika kabisa maana ubora wa maziwa toka shambani kwako ndio utakaokusadia katika kujipatia wateja wa kudumu. Katika biashara yoyote, mteja ndiyo injini ya biashara yenyewe,  hata uwe na mtaji mkubwa kiasi gani, biashara utakayoianzisha kama haitakuwa na wateja wa kutosha, biashara hiyo utaiendesha kwa hasara kubwa na mwisho itakufa. Ili kufanikisha biashara yoyote ni lazima bidhaa utakayozalisha iwe na ubora wa kipekee, na sana sana biashara ya chakula kwa sababu ladha ya chakula chochote haihitaji kupimwa kwa mashine isipokuwa inaonjwa kwa mdomo tuu. Maziwa yanatumika kwa namna mbalimbali, lakini pia yanatumika kama kinywaji yakiwa baridi kwa kuzima kiu, maziwa yatamfurahisha mnywaji kama yatakuwa yamekidhi viwango kama inavyopendekezwa na wataalam wa lishe.
          Hebu sasa tuangalie ni jinsi gani tunavoweza kuzalisha maziwa katika kiwango bora kabisa. Jambo la kwanza kabisa la kufanya ili kifikia malengo haya ni kuchagua jamii ya ng'ombe iliyobora katika uzalishaji wa maziwa,  zipo jamii nyingi za ng'ombe wa maziwa, itategemea wewe umechagua jamii ipi,ila ni vizuri ukapata ushauri  kutoka kwa mtaalam wa ufugaji, kama nilivyokwisha kusema tangia awali leo siyo siku ya kudadavua jamii zilizopo maana ni somo pana linalohitaji makala yake nzima. Ni muhimu na ni lazima kuchagua ng'ombe wa maziwa kutoka kwa mzazi mwenye sifa zinazotakiwa kwa ajili ya kuzalisha maziwa mengi na yaliyo mbora, kuna uchunguzi uliokwisha fanyika na kuthibitishwa kuwa ndama jike anarithi kwa mama yake kiwango cha maziwa atakachozalisha kwa siku, ndiyo maana katika kuchagua ng'ombe utakaofuga ni lazima ujiridhishe na historia ya mama yao au ukoo anakotokea.
          Jambo la pili ambalo ni muhimu kabisa pia ni juu ya chakula atakachokula tangu akiwa ndama mdogo hadi kuwa mtamba,na baadae wakati akiwa na mimba hadi wakati wa kukamuliwa , leo tutaangazia juu ya chakula atakachokula wakati ng'ombe akiwa na mimba na wakati wa kukamuliwa maziwa. Kipengele hiki ndicho kilichobeba kichwa cha mada yetu ya leo. Chakula bora ni chakula cha namna gani? Chakula bora ni kile chenye uwezo wa kujenga mwili wa ng'ombe mwenyewe,  maana ng'ombe anatakiwa kukua katika viwango vilivyokusudiwa, ng'ombe asipopata chakula bora na cha kutosha cha kujenga mwili, ng'ombe atadumaa na mwishowe hataweza kuzalisha maziwa mengi na yaliyobora, maana ukubwa wa mwili wa ng'ombe unatafsri wingi na ubora wa maziwa atakayozalisha.
KUKAMUA KWA KUTUMIA MASHINE.
            Hali kadhalka ng'ombe anatakiwa apatiwe chakula kitakachotia mwili joto, kutia nguvu mwilini na chakula kitachofanya mwili kuwa na uwezo wa kujikinga na maradhi. Mchanganyiko uliobeba vyakula hivyo vilivotajwa hapo juu ndio mlo kamili utaoweza kumfanya ng'ome aishi vizuri na kumfikisha mfugaji katika malengo yake. Kipindi cha miezi mnne tangu ng'ombe azae ndicho kipindi ambacho ng'ombe anatoa maziwa kwa kiwango cha juu cha uwezo wake, na hiki ndicho kipindi ambacho mfugaji anatakiwa awe makini sana katika kulisha ng'ombe wake, ng'ombe anatakiwa alishwe majani uzito wa asilimia kumi ya uzito wake wa mwili, kama  atakuwa na uzito wa kilo450,  basi anatakiwa kulishwa kilo 45 za majani machanga ya kijani kibichi kabisa,  majani haya yalishwe pamoja na majani makavu wastani wa kilo sita kwa siku, majani makavu yatasaidia kufanya uwiano katika tumbo la ng'ombe ili ng'ombe asipate choo laini sana,  majani machanga na ya kijani ndiyo yenye virutubisho vyote vinavyotakiwa kwa ngombe, majani makavu yanakuwa na kiwango kidogo sana cha viini lishe vinavyotakiwa na mnyama, hapa tuone chakula kamili cha ng'ombe mwenye mimba na yule anaekamuliwa maziwa.
             Majani mabichi 10% ya uzito wa mwili wake. Majani makavu kilo 6, kuhusu virutubisho vingine mhimu ni kilo mbili za mchanyiko wa vitu vifuatavyo,
1)Shayiri/Ngano                                              30 Kg
2)Paraza ya mahindi                                        34 Kg
3)Mashudu ya alizeti                                       11 Kg
4)Mashudu ua pamba                                      15 Kg
5)Soya                                                               8 Kg
6)Chumvi                                                        0.5 Kg  
7)Mchanganyiko wa madini maalum              1.5 Kg.
Jumla inakuwa                                              100 Kg.
           Mchanganyiko huu unatakiwa kuandaliwa katika mashine ya kusaga na kuchanganya chakula cha mifugo ili kupata matokeo mazuri, ni vizuri ukajiandaa ili utengeneze nusu tani au tani moja au zaidi kwa wakati mmoja ili upunguze ngarama za kusaga na kusafirisha, maana katika mashine nyingi za kuchanganyia vyakula huwa wanatoza kwa nusu tani au tani moja kuendelea, hivyo kama kwa mfano unataka kusaga na kuchanganya kilo 200, basi utatozwa pesa ya nusu tani.
         Ni muhimu sana sana kutumia mashine kuchanganyia chakula kuepuka matatizao aina moja ya chakula au chumvichumvi kulundikana mahali pamoja ambapo zinaweza kumdhuru ng'ombe au kuifanaya lishe isifanye kazi yake inavyotakikana, inawezekana pia kuchanganya kwa mkono lakini uangalifu na umakini viahitajika. Unaweza kuuliza katika hiyo list hapo juu Pumba ya mahindi haikutumika, kama nilivyokwishaeleza katika makala zilizopita kuwa ni mara chache sana unaweza kupata pumba iliyo salama. Machine nyingi za kukobolea mahindi zinaendeshwa katika hali isiyoridhisha kiusafi.
         Kiroba  kimoja cha pumba mbichi iliyokobolewa inafikia hadi elfu ishini na nne                   (Tshs 24,000)kiroba kimoja kipimo cha ujazo ni ndoo saba za lita ishirini, ukishafanya kazi ya kuikausha uzito uanabakia wastani wa kilo 60-70. ukigawa uzito kwa pesa za kununulia unapata bei ya kilo moja ni shilingi 343, ambazo kwa karibu sana zinalingana na bei ya kununulia kilo moja ya mahindi safi, kwa ushauri wangu naonelea ni afadhali kutumia mahindi kuliko kutumia pumba ambayo usafi na usalama wake unakuwa mdogo sana.
            Kufuga kwa mazoea kuna hasara nyingi sana, asilimia kubwa ya wafugaji wa wanyama wamegandisha mawazo yao katika kulisha mifugo yao PUMBA tu, akishajiwekea akiba yake ya pumba ya kutosha anapumzisha akili ana kustarehe akijiaminisha kuwa sasa wanyama wake watanawiri kwa kula PUMBA! Haikatazwi kulisha wanayama pumba, ila chanzo cha pumba yenyewe kiwe cha kuaminika, baadhi ya mahindi huhifadhiwa kwa kutumia dawa za kuzuia nafaka zisiharibiwe na wadudu, dawa hizi zikokatika jamii ya SUMU, hivyo kabla ya mahindi kutumika yanatakiwa yasafishwe vya kutosha, mimi siamini sana kama zoezi hili linafanyika ipasavyo katika baadhi ya mashine za kukobolea mahindi, na ni vigumu pia kugundua pumba yenye sumu hizi.
          Faida za kutumia mahindi safi ziko nyingi, wala hakuna haja ya kuzitaja hapa, kwa hiyo tujaribu sana kuondokana na kufanya ufujaji wetu kwa mazoea, badala yake tuangazie zaidi katika kufuga kitaalam, Nashauri uende Tandale, kuna wauzaji wengi wa mazao yatokayo mikoani, fanya nao mazungumzo jinsi unavyowe kupata mahindi, ngano,  mtamana kadhalka kwa ajili kwa ajili ya kulishia wanyama wako kwa bei nzruzi na nafuu, hawa pia wanaweza kukushauri miezi unayoweza kununua nafaka hizi kwa bei ya chini na kujiewekea akiba hata ya mwaka mzima na ukafurahia maisha ya ufugaji na kujipatia mazao mengi na bora.
        Maji ni sehemu muhimu sana ya chakula cha ng'ombe anayekamuliwa, inashauriwa ng'ombe apewe maji ya kutosha yaliyo safi na salama, maji yanatakiwa kuwa yanapatikana muda wote usiku na mchana, katika ufugaji wetu wa mazoeya tumezoea kuwapa ng'ombe maji pale tunaposikia wakilia au wakiashiria kutaka maji, hii si sawa kabisa, maji yawepo ya kutosha katika zizi la ng'ombe muda wote, mchana na usiku kabla ya kulala uhakikishe maji yapo ya kutosha kutumika usiku kucha. maji ni muhimu kuwepo zizini muda wote. 
       Kampuni ya Hydroponic Fodders Tanzania ni kampuni inayojiandaa kwa ajili ya kutatua tatizo la chakula cha mifugo yako, tunajiandaa katika kuhakikisha tunatatua tatizo la chakula cha mifugo yako kwa kukupatia mtiririko wa chakula cha kitaalam ambacho tuna uhakika kitainua mapato yako kwa asilimia hamsini(50 %) kama ng'ombe wako wanakupatia maziwa lita kumi, tuna uhakika wa kupandisha uzalishaji hadi lita ishirini, tena kwa gharama nafuu sana.
        Nakushukuru sana kwa kusoma makala yangu hii mwanzo hadi mwisho, nakutakia baraka za Bwana Mungu katika harakati zako za kujitafutia riziki halali, nikusihi sana usindoke bila kuacha maoni yako katika sanduku la maoni hapo chini.uliza maswali, toa maoni yako pia.Tukutane tena katika makala nzuri inayofuata, ni matumaini yangu kuwa utafaidika katika mtiririko wa makala hizi na utaweza kuongeza kipato chako kwa uhakika zaidi.
      UBARIKIWE NA BWANA MUNGU.
        

Maoni 15 :

  1. Nashukuru kwa elimu nzuri sn Mimi ni mfungaji Wa ngombe nipo mwanza naulizia wp mefikia ktk kuzalisha hicho cahakula ili tukipate kwa being nafuu sn

    JibuFuta
  2. Asante hii itanisaidia kuboresha mifugo yangu

    JibuFuta
  3. Haya majani mabichi nitayapataje kipindi

    JibuFuta
  4. Aisee mmetisha, nimependa sana elimu hiyo, hofu yangu ni juu ya upatikanaji wa hicho mtakachotengeneza kwa sisi tulio mbali nanyi Kgm

    JibuFuta
  5. Katika maeneo mengi kuna changamoto ya majani na hivyo virutubisho Ila nielimu Nzuri sana hongereni

    JibuFuta
  6. Safi Sana ni elimu tosha

    JibuFuta
  7. Elimu nzuri Sana naomba mwendelee kutupa ujuzi kazi nzuri Sana nime ipenda big up sana

    JibuFuta
  8. Asante elimu nzuri Mimi nahitaji msaada wa kazi kwani nina elimu juu ya mambo hayo nitashukuru kama utanisaidia

    JibuFuta
  9. Asante elimu nzuri Mimi nahitaji msaada wa kazi kwani nina elimu juu ya mambo hayo nitashukuru kama utanisaidia

    JibuFuta
  10. Nikikosa mashudu ya pamba je naweza jazia mashudu ya alizeti au italeta madhara

    JibuFuta
  11. Elimu yenu nimeipenda, nikiwa mbeya nawapataje, naamini kwenu nitapata elimu kubwa zaidi sana, simu yangu 0679166821

    JibuFuta