Nimejaribu kufanya uchunguzi na kubaini kuwa kuna fursa nyingi sana hapa nchini zinazo weza kutufanya tuishi maisha bora bil ashaka yoyote, fursa hizi zipo kutegemea na eneo ambalo mtu yupo, kwa mfano fursa zilizopo mjini ni tofauti na zinazopatikani vijijini.
Leo tuangazie fursa zilizopo katika miji au majiji yetu, katika miji zipo fursa nyingi sana, ila kwa leo tuangalie zile fursa ambazo tunaweza kuzitumia kufanya mabadiliko katika maisha yetu kwa mtaji mdogo, kuna fursa katika viwanda vidogo vidogo kuna fursa katika viwanda vya kati na vilevile viwanda vikubwa.
Ninapozungumzia mtaji mdogo ninaamaanisha mtaji ulio chini ya milioni kumi, labda tuangalie ni vipi tunavyoweza kutumia mtaji wa milioni nne. Mpaka kufikia hapa kuna mtu tayari ameanza kushtuka na kuanza kufikiri ni jinsi gani milioni nne inavyoweza kupatikana.
Ikiwa kama wewe ni msomaji mzuri wa makala za ujasiriamali utakubaliana na mimi kuwa yalisha fundishwa masomo na semina nyingi kuhusiana na jinsi unavyoweza kuanzisha biashara bila kuwa na chochote mkononi. Jambo hili linawezekana pale mtu unapokuwa umejipanga na kufanya maamuzi kutoka chini kabasa ya moyo wako.
Nasema maamuzi yawe ya moyoni na ya dhati kwa sababu kwa jinsi tulivyoumbwa na Mungu, tumejengewa dhamira ya dhati kabisa ndani mwetu yenye kichocheo kikubwa cha kutufanya tubuni miradi mingi yenye kutupeleka katika mafanikio kwenye maisha yetu.
Lakini pia ndani mwetu shetani hakosekani kila wakati, kaweka maskani yake ya kudumu akiwa tayari kung’oa yale mema yote ambayo Mungu ameweka ndani yetu. Kama mimi nilivyo, na wewe ukohivyo hivyo, kila wakati najiwa na mawazo mazuri ya kuanzisha biashara, nakaa chini napiga hesabu na kuona mwanga ukiangaza mbele kuelekea katika mafanikio.
Lakini badala ya kupiga moyokonde na kuanza kutekeleza yale mawazo mazuri niliyoyawaza, shetani hutokea mara moja na kuyafuta katika dhamira ya kweli ya moyo. hapa uvivu huchukua nafasi yake, shetani anapandikiza haraka sana mbegu ya kushindwa, mawazo ya kukata tamaa, mahesabu ya haraka jinsi utakavyopata hasara kubwa na mambo mengine mengi yaliyo hasi.
Ukishafikia hapa taratiibu unaanza kuliona wazo hili halifai na unaanza kubuni wazo jingine, kama nilivyosema hapa juu kuwa Mungu ni mwema kwetu siku zote, kajaza akilini mwetu maarifa na vipaji tele, ndiyo maana ukitoka kuwaza mradi huu, halafu ukauacha, Mungu hakawii kukuletea wazo jingine, ila kama awali habari ina kuwa ileile.
Sasa mjasirialimali mwenzangu, naendelea kukukaribisha katika jukwaa hili la kusaka maendeleo, tuanze kudema dema kidogo kidogo na mwisho tuweze kupata furaha kama Mungu alivyotaka tuishi katika dunia hii tukifurahia maisha kwa amani.
Kuna wataalam wengi sana waliokaa wakatumia bongo zao, wakaandika maandiko mengi mazuri katika Lugha laini na nyepesi, sisi kazi yetu ni kupata muda wa kufungua vitabu hivyo na kupakua chakula ambacho tayari kimeshaivishwa vizuri.
Lakini shetani hataki kutuacha tupakue vyakula hivi na kuvila kwa afya ya maendeleo yetu, mara zote amekuwa mwepesi wa kututia uvivu na mawazo mgando, na kwa ulaghai wake tumekuwa watiifu mno kwake. Unaweza kusikia matangazo mengi ya semina za bure,lakini badala ya kwenda katika semina hizo, utamkuta kijana akielekea katika kijiwe kwenda kuendelea kusikiliza hadithi pale ilipoishia jana.
Kama hatujafanya maamuzi ya busara kuanzia sasa, tutabakia kuwa watu wa kulialia mpaka mwisho wa maisha yetu bila kufurahia kile Mungu alicho tukusudia kufurahia hapa duniani, maana Mungu ametuwekea kila kitu tayari,kazi yetu ni kuvifanyia kazi na kuyafurahia maisha.
Mwaka jana kuelekea mwishoni kulifanyika semina moja nzuri sana sana,semina hii ambayo kila siku naiota moyoni mwangu ilikuwa ikifanyikia pale victoria petrol station, pale kwa juu kuna ukumbi ghorofani.
Semina hii nzuri sana iliendeshwa bure kwa taktban miezi miwili na Bwana Eric Shigongo, sina haja ya kumuelezea hapa Eric Shigongo ni nani,maana sidhani kama nina maneno kamilifu ya kumuelezea mtu huyu muhimu sana unapotaka kuzungumzia mambo ya ujasiriamali.
Ila ninaamini wengi wetu mnamfahamu kupitia njia mbalimbali ambazo kwazo anajidhirihisha,kwa kutaja machache tu, Magazeti yake pendwa , vitabu vyake vingi vinavyofundisha ujasiriamali katika lugha laini ya kueleweka na kila mtu,Dar Live Mbagala katika kisima cha burudani, na mambo mengine meengi anoyojihusisha nayo katika kujitolea kwa kuitumikia jamii yake.
Nasema semina hii naikumbuka na kuiota kwa mengi,kama wewe unayesoma hapa uliwahi kuhudhuria semani ile , ama kwa hakika utakubaliana na maneno yangu, semina hii ilikuwa inafanyika kila siku ya jumapili kuanzia saa nane hadi saa kuminambili jioni, ila muda huu wa masaa manne au matano hivi ulikuwa unapita kwa kasi sana.
kama binadamu wengine na huwa kuna mahali natamani kusikia mzungumzaji au tuseme mchungaji akisema tusimame tufunge ibada, lakini kamwe katika semina ile sikuwahi kuwaza vile, maana kila kitu kilikuwa kinafanyika kwa mpangilio wake,
Tulikuwa tunaaza semina yetu kama ibada,kufungua kwa sala,halafu tunaendelea na kusifu na kuabudu tukiongozwa na waimbaji wa kundi la GWT,ama kwa kusema ukweli kundi hili limesheni vijana walokole wenye ujuzi mkubwa wa kumsifu Mungu,wajuzi wa kupiga ala mbalimbali za muziki kwa umahiri wa hali ya juu kabisa.
Jamani tumwacheni Mwalimu Julius Nyerere akapumzike kwa amani. nasema hivyo kwa kuamini kazi aliyoitiwa kufanya duniani aliifanya kwa umakini na uaminifu mkubwa, nasema hivyo kutokana na umoja wa kindugu aliotujengea miongoni mwetu, maana katika semina yetu tulikuwa tunahudhuria wengi, vijana kwa wazee, watu wa dini zote, na hapa ndiyo kiini cha kupenda kumkumbuka Mwalimu Nyerere,alifanya kazi kubwa kutujengea tabia ya umoja.
Kusema kweli semina yetu ile ilielemea zaidi kuongozwa Kikristo, lakini kama nilivyotangulia kusema hapo juu kuwa mahudhurio yalikuwa ya watu wa dini zote sikuwahi kusikia malalamiko hata siku moja , hali ilikuwa shwari mwanzo hadi mwisho wa semina, nilifurahi sana kuona jambo lile likifanyika kwa amani, siyo rahisi kuona jambo kama lile likifanyika kwa amani vile katika mataifa mengine.
Nafikiri kuna mtu anaanza kujiuliza haya mambo ya semina yanatokea wapi katika makala haya, nimeyaandika haya ili kama utayasoma makala haya ujue kwamba ,yatakayofundishwa au kupatikana katika blog hii, kuwa ndiyo matunda ya semina ile,maana katika semina ile tulifundishwa mambo ya ujasiriamalli kwa mapana na marefu yake.
Nichukue pia nafasi hii kumshukuru sana Bwana Eric Shigongo na timu yake kwa ajili ya kutupatia semina ile, tena bure kabisa na zawadi ya kitabu chake chenye gharama ya shilingi elfu kumi bure kabisa, Bwana Mungu azidi kumzidishia mkate wake na amjaalie maisha marefu kwa kadri ya mapenzi yake(Bwana Mungu)
Pamoja na masomo mengi ya msingi sana ya elimu juu ujasiriamali tuliyofundishwa katika semina ile, somo la kujua ni Biashara gani ufanye ili uweze kuuza kwa wingi na kutengeza faida, ndilo somo lililo chimbuko la kuanzishwa blog hii ya “HYDROPONIC FODDERS TANZANIA”.Jina hilo pia litakuwa jina la kampuni yangu hapo nitakaposajili rasmi siku chache zijazo.
Wazo hili nimelipata takriban mwaka mmoja baada ya kumalizika kwa semina lie, maana baada ya kumalizika kwa semina ile nilipata bahati ya pekee ya kukaribishwa ofisini kwa Bwana Eric Shigongo na kuweza kakaa na kijadili ni kitu gani ningeweza kufanya kwa wakati ule.
Lakini kwa kweli nilipata kigugumizi ni nini ningeweza kufanya kwa wakati ule,maana ni muda mfupi sana niliobahatika kukaa na Bwana Eric Shigongo, nilijaribu kumwambia nina wazo hili au lile, hakuna hata moja lililokubalika mbele yake.
Kutokana na ufinyu wa muda wake na ratiba yake kubana sana, niliona tu yatosha kwa semina yake kwa wakati ule nimpishe afanye mambo yake huku nami nikajipange vizuri maana mtihani wa kubuni wazo jipya la biashara kama alivyobuni mwana semina mwenzetu, mradi wa kuzoa takataka kule Kigamboni halikuwa jambo jepesi sana.
Walau nami naanza kupata furaha juu ya wazo la kuanzisha biashara ya kutatua tatizo la MALISHO ya wanyama wetu katika jiji la Dar es salaam,malisho maridhawa kabisa kwa ng’ombe wa maziwa na wanyama, nguruwe na kuku kwa gharama nafuu sana.
Malisho haya ya majani yenye virutubisho karibu vyote muhimu kwa mfugo wetu,yatapatikana kwa urahisi, nina maanisha kuwa mfugaji atapata malisho ya mifugo yake kwa muda mwafaka kabisa,baada ya mfugaji kuingia mkataba maalum na kampuni yetu,na kutulipa kwa kadri ya makubaliano yetu,
Kazi ya kampuni ni kuhakikisha mfugaji anapata malisho ya wanyama wake kama mkataba utavyosomeka, kazi ya mfugaji itabakia kufurahia huduma yetu tuu.
Nawakaribisha katika makala inayofuata, naomba maoni yako tafadhali, masahihisho pia kwa pale nilipokesea maana hizi ni makala zangu za mwanzo kabisa katika kuandikia blog yangu. Nakushukuru sana WEWE uliyesoma makala haya tangu mwanzo hadi mwisho.
Naomba Bwana Mungu akubariki kwa kadri ya mapenzi yake yeye mwenyewe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni